Shirika la Kilifi Citizen Forum limekiri kwamba ukosefu wa ajira kwa vijana kaunti ya Kilifi ndio chanzo cha kuchipuka kwa visa vya mauaji ya wazee kwa tuhma za uchawi.
Afisa wa masuala ya vijana katika Shirika hilo Ishmael Jilani alisema kuna haja ya mikakati mwafaka kuidhibishwa na serikali kuu na kaunti ya Kilifi ili kudhibiti visa hivyo.
Jilani, amesema japo visa hivyo vimepungua kwa asilimia kubwa bado kuna haja ya hamasa za mara kwa mara kwa jamii mashinani pamoja na mikakati ya ajira kwa vijana kwani hatua hiyo inarudisha nyuma juhudi za maendeleo.
Aidha alidai kuchukizwa na jinsi vijana wengi wanavyowachukulia wazee kama watu wasiokuwa na thamani katika jamii, akisema wazee wana mchango kubwa hasa kwa ushauri, maarifa , hekima na pia wamekuwa mstari wa mbele katika kuelekeza serikali hasa kwenye masuala ya mipaka ya mashamba.
“Visa vya mauaji ya wazee vimetokana na vijana kukosa ajira na kutaka kutumia raslimali za wazee kujiendeleza na hapo ndio tatizo maana wazee wanahusishwa na tuhma za uchawi, tumejaribu sana kuhamasisha jamii ndiposa hivyo visa vimepungua lakini ni lazima serikali kuu na kaunti ya Kilifi kubuni ajira kwa vijana”, alisema Jilani.
Wakati huo huo aliwarai vijana kujitenga na hulka hizo na badala yake kuwa wabunifu wa ajira na kuwaheshimu wazee kwani wana mchango mkubwa kwa jamii.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi