Entertainment

Ndoa Tano Tena: Ruby Kache Asitisha Mpango wa Ndoa kwa Miaka Mitano

“Nitangoja tena miaka mitano kabla sijafanya maamuzi ya kuolewa.” — Ruby Kache

Published

on

Mtangazaji wa kipindi cha The Wave, Ruby Kache, amefunguka kwa hisia kali kuhusu maamuzi yake ya ndoa — akisema kuwa atasubiri miaka mingine mitano kabla hajafanya uamuzi wowote kuhusu kuolewa.

Katika mjadala moto uliotikisa hewani kati yake na mtangazaji  mwenzake Hon. Baba Yaga, Ruby alieleza kuwa kauli ya Baba Yaga kwamba “mpango wa kando ni lazima katika ndoa” ilimvuruga sana na kumfanya arejee upya mtazamo wake kuhusu taasisi ya ndoa.

“Ndoa tano tena,” alisema Ruby.

Kauli ya ulizima wa mchepuko kwenye ndoa inaonesha jinsi taasisi ya ndoa inavyochukuliwa kwa mzaha. Na labda miaka mitano ni muda wa kutosha kwa Ruby kutafakari, na kujiandaa kwa maamuzi makubwa ya kuolewa.

Kauli hii ilitolewa wakati walikuwa wakichambua kisa cha mwanamume aliyemwandikia mpango wake wa kando ujumbe akimweleza kuwa matatizo ya uhusiano wao huathiri hata ndoa yake rasmi.

Katika maelezo yake ya kulinda mtazamo wa mwanaume huyo, Baba Yaga alitoa mfano tata akisema:

“Kama serikali inahitaji upinzani ili iwe na mwelekeo, basi hata ndoa inahitaji mpango wa kando ili iwe na mizani.”

Kauli hiyo ilizua sintofahamu, mshangao kwa Ruby Kache ambaye alitafsiri maneno hayo kama kejeli kwa taasisi ndoa.

Kipindi hicho kiligeuka kuwa jukwaa la kuibua maswali mazito kuhusu hali ya mahusiano na ndoa katika kizazi cha sasa — haswa kizazi cha Gen Z. Ni kweli kwamba kwa wengi wao, ndoa haionekani tena kama hitaji la lazima, bali kama chaguo la mwisho. Ruby alisisitiza kuwa hawezi kuwa sehemu ya maamuzi yenye msingi dhaifu wa kimaadili.

“Tunaishi wakati ambapo maadili yanapotea. Mapenzi yamegeuka bidhaa. Siwezi kuingia kwenye ndoa kwa sababu tu ni wakati au umri wangu. Nataka kuingia nikiwa na uhakika,” alisema Ruby kwa msimamo.

Jambo moja lililo wazi ni kwamba mjadala huu haujaisha. Katika jamii inayokumbwa na mabadiliko ya kitabia, kiuchumi na kiutamaduni, mtazamo wa vijana kuhusu ndoa unaendelea kubadilika. Je, kuchelewa kuoa au kuolewa ni hekima au hofu? Je, ndoa bado ni taasisi takatifu au ni tu mkataba wa kijamii usio na thamani ya kihisia?

Kwa Ruby Kache, jibu ni wazi: si kila mtu anahitaji ndoa haraka, na si kila ndoa ni salama. Muda ni kigezo muhimu cha kuamua mustakabali wa maisha ya wawili.

The Wave hurushwa kila Jumamosi kuanzia saa 4 asubuhi hadi saa 7 mchana kupitia Coco FM, ikiongozwa na Ruby Kache, Hon. Baba Yaga na Dj Capuchino. Kipindi hiki kinaendelea kuvutia maelfu ya wasikilizaji kwa mijadala yake ya ukweli, yenye kuchokoza fikra.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version