News

Mwili wa marehemu Samuel Kirao wafukuliwa

Published

on

Hatimaye familia ya Marehemu Samuel Kirao Charo imepata haki ya kuuzika mwili wa mpendwa wao baada ya mzozo uliokuwepo hapo awali na kupelekea marehemu kuzikwa kwa mujibu wa dini ya Kiislamu.

Hii ni baada ya familia hiyo kushinda kesi kwenye Mahakama ya Malindi wakati ambapo Mahakama ya Kadhi ilikuwa imeidhinisha jamii ya Waislamu kuuzika mwili huo kwa msingi kwamba Marehemu alikuwa muislam hata wakati wa kufa kwake.

Jaji Mugure Thande wa Mahakama ya Malindi alitoa uamuzi wa kufukuliwa kwa mwili huo na kisha ukabidhiwe familia yake ili uzikwe upya baada ya familia kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama ya Kadhi.

Eunice Kirao ambaye ni mama mzazi wa marehemu alisema marehemu alisilimishwa akiwa na akili punguani, akieleza kusikitishwa na jamii hiyo ya waislamu kutowapatia nafasi na badala yake ikashurutisha ibada ya mazishi kwa nguvu.

Kwa upande wake babake marehemu Stephen Kirao alisema wamepitia gharama nyingi za kuandaa mazishi kabla ya jamii ya waislamu kuuzika mwili wa marehemu, akisisitiza kuwa ni sharti gharama hizo zilipwe.

Familia ya Marehemu Samuel Kirao Charo katika makaburi ya Takaungu

Naye Kalume Charo ambaye ni kakake mkubwa marehemu alieleza kwamba hali haijakuwa nzuri muda wote huo kwani wamekuwa wakipitia kejeli na unyanyapaa katika eneo wanaloishi mbali na wazazi wao kuathirika kiafya.

Ikumbukwe kwamba marehemu Samuel aliuawa na umma baada ya kumuua kwa kumdunga kisu Ustadh mmoja eneo la Takaungu na kisha kuula utumbo wake.

Taarifa ya Hamis Kombe

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version