National News
Mweni: Gavana Mung’aro Anafaa Kuwa Makini na Baadhi ya Viongozi
Mwakilishi wadi ya Sokoke kaunti ya Kilifi Thaura Mweni ameibua madai kwamba kuna vijana ambao walilipwa kima cha shilingi elfu 50 ili kuzua vurugu katika mkutano uliofanyika eneo la Matano mane wakati wa hafla ya mashindano ya usomaji wa Quran mwishoni mwa juma.
Akizungumza na CocoFm, Mweni amesema vijana hao walilipwa ili kuzua vurugu dhidi yake kwa kile kinachoonekana kuwa tofauti za kisiasa baina yake na baadhi ya viongozi wanaoaminika kuwa wandani wa Gavana wa kaunti ya Kilifi Gideon Mung’aro.
Mweni amesema kwamba haina haja ya malumbano ya kisiasa bali ni vyema iwapo kutakuwa na ushirikiano baina ya viongozi wa kaunti ya Kilifi kwa manufaa ya wakaazi.
Wakati huo huo amepuuzilia mbali matamshi ya kiongozi wa wengi katika bunge la kaunti ya Kilifi Ibrahim Matumbo, akisisitiza haja ya Gavana Mung’aro kuwa makini na viongozi anaoshirikiana nao.