News

Mahakama ya Malindi yawaachilia washukiwa 3 wa kesi ya Kwa Binzaro

Published

on

Mahakama Kuu ya Malindi imewaachilia washukiwa watatu wanaohusishwa na kesi ya mauaji ya halaki ya watu katika kijiji cha Kwa Binzaro eneo bunge la Magarini kaunti ya Kilifi.

Hakimu wa Mahakama hiyo Joy Wesonga aliagiza kuachiliwa huru kwa Safari Kenga Nzai, Gona Charo Kalama na Kahindi Kazungu Garama wote wakiwa wakaazi wa kijiji hicho cha Kwa Binzaro.

Watatu hao walikuwa wamekamatwa baada ya kudaiwa kuuza shamba la ekari tano kwa mshukuwa mkuu wa mauaji ya watu katika kijiji cha Kwa Binzaro Sherleen Temba Anido.

Hakimu Wesonga aliwaagiza washukiwa hao kuhakikisha wanasalimisha nakala za vitambulisha vyao vya kitaifa kwa idara husika, kuripoti kwa Naibu Chifu wa eneo hilo mara mbili kwa wiki pamoja na kujisalimisha kwa maafisa wa upelelezi wa kesi hiyo mara moja kila baada ya wiki mbili.

Miili iliyofukuliwa katika kijiji cha Kwa Binzaro 

Wakati huo huo upande wa mashtaka ukiongozwa na Naibu mkurugenzi wa mashtaka ya umma Jamie Yamina, uliomba kuwasilisha watu wengine wanne Mahakamani ikiwemo Jairus Otieno na mkewe Lilian Akinyi, Kahonzi Katana Karisa na Loise Zawadi waliojionda kama washukiwa na kugeuka kuwa mashahidi wa serikali.

Upande wa mashtaka pia uliaka kupewa siku 60 zaidi kuendelea kuzuiliwa kwa washukiwa wakuu Sherleen Temba Anido, James Kahindi Kazungu, Thomas Mukunwe na Kahidi Kazungu Garama katika kituo cha polisi cha Ngerenya, Kilifi, Watamu na Kijipwa ili kukamilisha uchunguzi wao kwani wanne hao wanakabiliwa na mashtaka ya itikadi kali, ugaidi, kujihusisha na uhalifu na kupanga mauaji.

Taarifa ya Mwahoka Mtsumi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version