News

Mhubiri mwenye utata Gilbert Deya ameaga dunia

Published

on

Mhubiri mwenye utata Gilbert Deya ameaga dunia baada ya kuhusika kwenye ajali ya barabarani katika eneo la Namba-Kapiyo kwenye barabara ya Bondo-Kisian maeneo ya Nyanza ajali ambayo imeacha watu wengine 30 na majeraha.

Kulingana na Kamanda wa trafiki eneo la Nyanza Peter Maina, ajali hiyo imehusisha magari matatu likiwemo gari la chuo kikuu cha Moi, gari la kaunti ya Siaya aina ya Toyota Fortuner na lengine Toyota Noah.

Maina alisema dereva wa gari aina ya Toyota Noah, lililokuwa likielekea eneo la Kisian sehemu za Bondo alipoteza mwelekeo na kugonga basi la chuo kikuu lililokuwa likielekea Kisumu.

Aidha alidokeza kwamba mhubiri Deya alikuwa akiendesha gari hilo aina ya Toyota Noah na alikuwa amebeba abiria wawili Wanawake mmoja akiaminika kuwa mkewe ambao wamepata majeraha madogo.

Wanafunzi 15 waliokuwa kwenye basi la chuo kikuu wamepata majeraha mabaya na wengine 15 wakapata majeraha madogo.

Mwili wa Deya ulichukuliwa na kuhifadhiwa katika makafani ya hospitali ya kaunti ndogo ya Kombewa huku baadhi ya majeruhi wakitibiwa katika hospitali hiyo na wengine katika hospitali ya rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga.

Taarifa ya Joseph Jira

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version