International News
Matumaini ya kusitisha vita Gaza yaanza
Licha ya Rais wa Marekani Donald Trump kusema kwamba mpango wa usitishaji mapigano kwa siku 60 katika Ukanda wa Gaza unakaribia, kundi la Hamas limeeleza kwamba bado mazungumzo yanaendelea.
Katika kile kinachoonekana kama jibu la kwanza la Hamas tangu Rais Trump kutangaza kupatikana kwa mwafaka huo, kundi hilo lilisema kwamba bado linaendelea kuyatafakari mapendekezo mapya yaliyomo kwenye mpango huo.
“Tunalichukulia suala hili kwa uangalifu mkubwa. Tunafanya majadiliano ya kitaifa kuyatathmini mapendekezo ya ndugu zetu wapatanishi”, lilisema kundi hilo kupitia Kiongozi wao.
Mnamo siku ya Jumanne Julai mosi mwaka huu, Rais wa Marekani Donald Trump alisema kwamba Israel ilikuwa imekubaliana na masharti ya kusitisha mapigano kwa siku 60 wakati mauaji kwenye ukanda wa Gaza yakiwa kwenye mwezi wake wa 21.
Trump alidai kwamba Misri na Qatar, ambazo ni wapatanishi wakuu, walikabidhiwa jukumu la kuwafikishia mapendekezo hayo Hamas lakini wakati huo huo akilitishia kundi hilo kutokuutakaa mpango huo.
“Tunaamini kwamba Misri na Qatar wanaendelea na mpango mzuri wa upatanisho na suala hili linafaa kuchukuliwa kwa uzito zaidi lakini pia ni lazma Hamas iwe waangalifu na kuzingatia masharti hayo”, alisema Trump.

Baraza la usalama lajadili upatishi Gaza.
Waziri wa Mambo ya nje wa Israel, Gideon Saar, alisema sehemu kubwa ya mawaziri kwenye serikali ya nchi yake wanaunga mkono makubaliano hayo ambayo yanajumuisha kuachiliwa kwa mateka.
Waziri huyo wa mambo ya kigeni aliongeza kwamba sehemu kubwa ya raia wa Israel wanaunga mkono makubaliano hayo kama inavyothibitishwa na uchunguzi wa maoni.
Hata hivyo, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anatarajiwa kukutana na Rais Trump wiki ijayo mjini Washington, ili kuangazia zaidi mikakati na mipango ya kudhibiti.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi