Sports
Kenya Harlequins Tayari Kwa Msururu wa Chistie 7s Nairobi
Kocha Mkuu wa kilabu ya Kenya Harlequins na mchezaji wa zamani wa Shujaa, Samuel Odongo, ameonya kuwa wako tayari kwa vita wakati wa toleo la 59 la Christie 7s litakaloanza hii leo, Agosti hadi 17 katika uwanja wa RFUEA.
Baada ya msururu wa Prinsloo Sevens,kikosi hicho kimepangwa Kundi A wakiwa pamoja na mabingwa wa Prinsloo mara mbili mfululizo, Strathmore Leos, Zetech Oaks na MSC Rugby.
Harlequins, ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya saba kwenye msururu wa National Sevens wakiwa na pointi 24, wameweza kumaliza katika nafasi ya sita kwenye Driftwood na Prinsloo Sevens. Odongo, anayelenga kutetea taji la jumla la Quins, alibainisha kuwa ushindani utakuwa mkali, hasa ikizingatiwa kwamba migawo miwili ya mwanzo tayari imetoa mabingwa tofauti na pia kuongezwa kwa kikosi maalum cha Uganda, Ruga Ruga.
“Mashindano haya yatakuwa magumu. Migawo miwili iliyopita imeshuhudia mabingwa wawili tofauti, na pia kuwa na Ruga Ruga kunaleta upekee wa aina yake. Itakuwa wikendi yenye msisimko wa kupanda na kushuka, hasa kwa timu kubwa kushangazwa, na tunatumai hatutajikuta kwenye kapu hilo,” alisema Odongo.
Kauli yake iliungwa mkono na nahodha wa Quins na nyota wa zamani wa U-20, Richel Wangila, ambaye alionyesha kujiamini licha ya mwanzo wa msimu usio wa kuridhisha.
“Tumeendelea kujijenga na kuwa wavumilivu. Hata baada ya matokeo yasiyoridhisha kwenye misururu miwili ya mwanzo, tuko tayari kuwapatie mashabiki burudani ya kuvutia. Tunakazana kushinda mchezo wa kwanza, kisha kuchukua kila mechi inavyokuja, huku lengo kuu likiwa ni kufika fainali na kulinyakua kombe,” alisema Wangila.
Mashindano hayo ya siku tatu yanaanza leo kwa michuano ya vijana asubuhi, ikifuatiwa na mashindano ya wastaafu jioni. Hatua kuu ya Christie Sevens inaanza kesho, ambapo inatarajiwa kushuhudiwa mchezo wa kasi wa raga huku timu zikipambana kwa alama muhimu za msururu.