Trump asema Marekani itasitisha vita dhidi ya Iran

Trump asema Marekani itasitisha vita dhidi ya Iran

Rais Donald Trump amesema kwamba Marekani itaondoka Iran hivi karibuni na hatua za kijeshi za nchi hiyo zitakomeshwa ndani ya wiki mbili au tatu zijazo.

Rais Trump alisema Marekani imefikia malengo iliyojiwekea kabla ya kuanza kwa mashambulizi ya anga dhidi ya Iran mwezi uliyopita kwa ushirikiano na Israel.

Aidha aliongeza kuwa lengo la kuizuia Iran kuwa na uwezo wa kuunda silaha za nyuklia limefikiwa na sasa Marekani inamaliza kazi.

Trump pia aliema Marekani sasa inatawala anga za Iran na pia imepata mabadiliko ya utawala kufuatia mauaji ya viongozi wakuu wa kisiasa na kijeshi.

Aliwataja viongozi hao wapya mjini Tehran kama walio na misimamo mikali na waadilifu zaidi, ikilinganishwa na watangulizi wao.

Trump pia alisema viongozi wa Iran wanaomba kufanya makubaliano na Marekani ili kumaliza vita, madai ambayo hapo awali yalipingwa na Iran na kuongeza kwamba vita vinaweza kumalizika bila makubaliano kati ya pande hizo mbili.

Kuhusu athari za vita hasa kupanda kwa bei ya mafuta, rais Trump alisema bei itashuka mara tu Marekani itakapomaliza hatua zake za kijeshi.