Idara ya usalama kaunti ya Kilifi imetoa onyo kali kwa wanaoendeleza unyakuzi wa ardhi za umma, ikisema watakabiliwa kikamilifu.
Kamishna wa kaunti ya Kilifi David Wanyonyi ametoa onyo hilo, akizidi kulionya kundi la Team Mashamba dhidi ya tabia hiyo.
Katika kikao na Wanabahari kuhusu usalama wa kaunti ya Kilifi kabla ya ziara ya rais William Ruto ya uzinduzi wa miradi ya maendeleo, Wanyonyi amesema serikali haitalinyamazia suala hilo wakati wananchi wakiendelea kuhangaishwa.
Kamishna Wanyonyi alisema tayari maafisa wa usalama wako nyanjani kuhakikisha usalama unaimarishwa kabla ya ziara ya rais, akiwataka wananchi kuondoa wasiwasi kwani maafisa wa usalama wako imara kulinda mali na raslimali za wananchi.
“Kama maafisa wa usalama tunatoa onyo kwa wavamizi wa mashamba ya umma wakidhani hayatumiki, tunawaambia hiyo tabia waache, hasa hii Team Shamba imekuwa na tabia ya kuvamia mashamba na kugawa, tunawaambia hiyo tabia hatutakubali na kutawakamata”, alisema Wanyonyi.
Aidha alisisitiza kwamba maafisa wa usalama hawatarudi nyuma katika kupambana na walanguzi wa dawa za kulevya kaunti ya Kilifi, akisema watakamatwa na kufikishwa Mahakamani ili kulinda vijana dhidi ya Mihadarati.
“Ni kweli kumekuwa na kesi za Mihadarati, lakini tunasema kwamba kama maafisa wa usalama kwa ushirikiano na vitengo mbalimbali tutahakikisha walanguzi wa Mihadarati wamekamatwa na kufikisha Mahakamani kulingana na sheria’,alisisitiza Wanyonyi.
Ziara ya rais Ruto kanda ya Pwani inatarajiwa kuwa na manafaa makubwa kwa wananchi, huku suala tata la ardhi, likitarajiwa kuangaziwa na wananchi kupewa hati miliki.
