Baada ya serikali na wadau wa sekta ya uchukuzi nchini kufikia makubaliano ya kusitishwa kwa mgomo wa kitaifa, sasa mikakati ya kupunguzwa kwa bei ya mafuta nchini imeenza.
Hatua ya kwanza na kukabiliana na hali hiyo ni kupunguzwa kwa bei ya mafuta ya Dizeli kwa shilingi 10 kwa lita na kuchangia bei mpya ya mafuta ya Dizeli kuwa shilingi 232.86 kwa lita katika jiji la Nairobi huku bei ya mafuta ya petroli ikisalia kuwa shilingi 214.25 kwa lita.
Katika jiji la Mombasa, bei mpya ya mafuta ya Dizeli itakuwa shilingi 229.58 kwa lita, mafuta ya petroli yakisalia kuwa shilingi 211.09 kwa lita huku mafuta ya taa yakipanda kwa shilingi 188.09 kwa lita.
Hata hivyo mjini Kilifi, bei mpya ya mafuta ya Dizeli itakuwa shilingi 230.45 kwa lita, mafuta ya petroli yakisalia kuwa shilingi 211.90 kwa lita na mafuta ya taa yakipanda kwa shilingi 188.96 kwa lita.
Sasa wadau hao wa sekta ya uchukuzi nchini wako na matumaini ya kupunguzwa zaidi kwa bei hizo za mafuta nchini katika kikao kinachotarajiwa kuandaliwa siku ya Ijumaa kati yao na rais William Ruto ili kuibuka na mwafaka wa suala hilo tata.
