Kumbukumbu za muaji ya kimbari Rwanda

Kumbukumbu za muaji ya kimbari Rwanda

Ni miaka 32 tangu kutokea kwa mauaji ya kimbari nchini Rwanda.

Leo, tarehe saba Aprili, raia wa Rwanda pamoja na dunia kwa ujumla wanaungana kukumbuka kuanza kwa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, ambapo zaidi ya watu laki nane, wengi wao wakiwa jamii ya Watutsi, waliuawa ndani ya kipindi cha siku mia moja.

Tarehe hii ni ya kihistoria kwa taifa hilo ambalo miaka 32 iliyopita lilikumbwa na moja ya matukio ya kikatili zaidi katika historia ya mwanadamu.

Mauaji hayo yalichochewa na kuuawa kwa aliyekuwa rais wa Rwanda Juvenal Habyarimana, tukio lililosababisha kuzuka kwa vurugu kote nchini.

Kilichofuatia ni mashambulizi ya kimbari kati ya Wahutu na Watutsi, ambapo zaidi ya watu milioni moja wanaripotiwa kupoteza maisha katika muda wa siku mia moja.

Wanawake, wanaume na watoto walilengwa katika mashambulizi hayo yaliyopangwa, jamii zikivunjika na dunia ikishuhudia tukio hilo kwa muda bila kuchukua hatua za haraka kuzuia maafa hayo.

Katika kuadhimisha siku hii, inayojulikana kama KWIBUKA, yenye maana ya “tunakumbuka,” bendera nchini Rwanda zinapepea nusu mlingoti, huku Rais Paul Kagame akitarajiwa kuwasha mwenge wa kumbukumbu katika makavazi ya Kigali.

Hata hivyo, licha ya historia hiyo ya maumivu, Rwanda imepiga hatua kubwa katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita, ikijijenga upya kutoka jamii iliyogawanyika hadi kuwa taifa lenye umoja, likishuhudia maendeleo ya kijamii na kiuchumi pamoja na juhudi za maridhiano na haki kwa wahanga.

Leo hii, Rwanda inasimama kama mfano kwa mataifa mengine aduniani, huku wito wa kuhakikisha mauaji ya kimbari hayajirudii tena ukiendelea kusisitizwa.

Taarifa ya Hamis Kombe