Mshukiwa wa ulanguzi na usafirishaji wa watoto anyimwa dhamana

Mshukiwa wa ulanguzi na usafirishaji wa watoto anyimwa dhamana

Mahakama ya Shanzu imemnyima dhamana mshukiwa wa ulanguzi wa watoto zaidi ya 20.

Mahakama imeagiza mshukiwa huyo kuzuiliwa rumande ili kuwawezesha maafisa wa polisi kukamilisha uchunguzi wao.

Mahakama imeelezwa kwamba mshukiwa huyo Almasi Rama Amos mwenye umri wa miaka 27 alikamatwa na maafisa wa upelelezi kutoka kitengo cha kupambana na ulanguzi wa binadamu na ulinzi wa watoto (AHTCPU) pamoja na maafisa wa idara ya upelelezi wa Jinai kutoka kaunti ya Mombasa.

Kukamatwa kwake kufuatia wiki kadhaa za uchunguzi kuhusu ripoti za unyanyasaji wa watoto zinazowalenga wasichana wadogo walio katika mazingira magumu.

Rama, anayetuhumiwa kwa kujihusisha na kundi linalodaiwa kuwa la ulanguzi wa watoto na dhulma za kingono na kufikishwa katika Mahakama ya Shanzu kufuatia operesheni ya kiusalama iliyoidhinishwa na maafisa hao.

Rama alipatikana katika mtaa wa Nguu Tatu eneo la Concordia katika kaunti ndogo ya Kisauni akiwa na watoto watatu wa kike.

Mahakama imeelezwa kuwa mshukiwa anadaiwa kuendesha “vituo vya uokoaji” katika kaunti za Mombasa na Kilifi kwa kujifanya kuwalea na kuwapa ushauri.

Kulingana na uchunguzi vituo hivyo vilikuwa vikitumika kama msingi wa dhulma za kingono na unyanyasaji wa watoto.

Alipokamatwa, mshukiwa aliwaongoza maafisa hadi kituo chengeni eneo la Ribe katika eneo bunge la Rabai, ambapo maafisa wa upelelezi waliwaokoa watoto 19 wa jinsia ya kike na kufikisha jumla ya waathiriwa waliookolewa kufikia ishirini na wawili (22).

Mbele ya Mahakama ya Shanzu tarehe 21 Mei, 2026, mshukiwa amekabiliwa na mfululizo wa mashtaka, ikiwemo unajisi, biashara ya watoto kwa madhumuni ya kuwadhulumu kingono pamoja na unyanyasaji wa watoto ambapo amekana mashtaka hayo.

 Kesi hiyo imepangwa kutajwa Juni 8, 2026.

Taarifa ya Teclar Yeri