Bunge la Israel limepitisha sheria mpya ya adhabu ya kifo

Bunge la Israel limepitisha sheria mpya ya adhabu ya kifo

Bunge la Israel limepitisha sheria mpya inayotoa adhabu ya kifo kwa Wapalestina watakaopatikana na hatia ya mashambulizi ya mauaji dhidi ya Waisrael.

Sheria hiyo ilipitishwa kwa kura 62 dhidi ya 48, huku mbunge mmoja akijizuia kupiga kura na wengine kutohudhuria kikao hicho.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alihudhuria kikao hicho na kupiga kura kuunga mkono mswada huo bungeni.

Mswada huo wa sheria uliwasilishwa na Waziri wa usalama wa taifa hilo Itamar Ben Gvir, ambaye ni mmoja wa wanasiasa wenye msimamo mkali nchini humo.

Hatua hiyo imeibua mjadala mkubwa wa kimataifa, huku mataifa ya Umoja wa Ulaya na mashirika ya haki za binadamu yakielezea wasiwasi mkubwa.

Muda mfupi baada ya kupitishwa, kundi la haki za binadamu la Israel lilisema limewasilisha malalamiko katika Mahakama kuu ya nchi hiyo.

Mamlaka ya Palestina ilitaja mswada huo kama uhalifu wa kivita dhidi ya watu wa Palestina, ikisema kwamba unakiuka mkataba wa Geneva.

Hata hivyo mamlaka ya Washington ilisema kwamba Israel ina haki ya kutungu sheria zake huku nchi zikiwemo Ujerumani, Ufaransa, Italia na Uingereza zikielezea wasiwasi mkubwa kuhusu mswada huo.