Ethekon: Uchaguzi mkuu utakuwa huru, haki na uwazi

Ethekon: Uchaguzi mkuu utakuwa huru, haki na uwazi

Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC imeanza rasmi zoezi la kuwasajili wapiga kura wapya kote nchini, huku ikilenga kuwasajili wapiga kura milioni 6.2, kabla ya uchaguzi mkuu ujao.Ā 

Mwenyekiti wa Tume hiyo Erastus Ethekon aliwahakikishia wakenya kwamba makamishna wa tume hiyo watahakikisha uchuguzi mkuu ujao unakuwa huru, haki na uwazi.

Akizungumza katika kaunti ya Kwale wakati wa kuzindua wa zoezi la usajili wa wakipiga kura kote nchini, Ethekon alisema serikali imewekeza raslimali za kutosha za kufanikisha zoezi hilo.

“Nataka kuwahakikishia wakenya kwamba tumejipanga kama IEBC na tuko na raslimali za kutosha kuhakikisha zoezi la usajili wa wapiga kura linaendeshwa vyema na uchaguzi mkuu utakuwa huru, haki na wazi ili kuhakikisha wakenya wanatekeleza jukumu lao la kidemokrasia na hatua hiyo tutafikia idadi ya wapiga kura zaidi ya milioni 27”, alisema Ethekon.

Naye Naibu Mwenyekiti wa IEBC Fahima Araphat alisema tayari maafisa wapya wa IEBC elfu 12 wameajiriwa kuhakikisha zoezi hilo liendeshwa vyema ili kusajili idadi kubwa ya wapiga kura

“Sisi tunafanya kazi yetu bila kuegemea upande wowote wa kisiasa na tuko tayari kuhakikisha anashinda uchaguzi anatangazwa mshindi kwa haki, na kama tuko na makarani elfu 12 na wote wasajili wapiga kura wapya elfu 10 kila moja tutakuwa na idadi kubwa ya wapiga kura, sasa hiyo ndio tunalenga kupata”, alisema Fahima.

Kwa upande wake Gavana wa kaunti ya Kwale Fatuma Achani, aliipongeza tume hiyo kwa zoezi hilo endelevu la wapiga kura, akisema ni hatua ya kipekee kwa jamii ambazo zimekosa fursa ya kujisajili kama wapiga kura.

Taarifa ya Mwahoka Mtsumi