Zoezi endelevu la usajili wa wapiga kura kote nchini limeng’oa nanga huku maafisa wa Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC wakilenga idadi kubwa ya vijana katika zoezi hilo.
Katika kaunti ya Kilifi eneo bunge la Kilifi Kazkazini, zoezi hilo limefanyika katika vituo vinne tofauti huku idadi ndogo ya wapiga kura ikishuhudiwa licha ya vuguvugu la TUKO KADI kuanzishwa na vijana ili kuwajisajili wapiga kura.
Akizungumza na Wanahabari wakati wa zoezi hilo, Naibu Afisa wa usajili wa wapiga kura katika eneo bunge la Kilifi Kazkazini Abdul Mohammed aliwarai vijana kujitokeza kwa wingi na kujisajili.
Mohammed pia aliwarai vijana kukoma kutumiwa vibaya na wanasiasa kwa manufaa yao binafsi, akipongeza vuguvugu lilionzishwa na vijana la TUKO KADI kama njia moja ya kuwahamasisha vijana kujisajili kama wapiga kura.
“Tumeanza zoezi hili na tunawahimiza vijana wajitokeze kwa wingi na kujisajili kama wapiga kura ili kutumia nafasi hiyo kuchagua viongozi wanawataka na wala wasikubali kutumiwa vibaya na wanasiasa”, alisema Mohammed.
Kwa upande wao baadhi ya vijana waliojisajili waliwarai vijana wenzao kujitokeza kwa wingi na kushiriki zoezi hilo ili kuchagua viongozi wanaohisi wataleta maendeleo sawa na kubuni nafasi za ajira.
Taarifa ya Elizabeth Mwende
