News

IEBC kufafanua mda mwafaka wa kampeni za uchaguzi

Published

on

Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC Erastus Ethekon ametangaza mipango ya kushauriana na mwanasheria mkuu wa serikali ya Kenya ili kufafanua kipi kinajumuisha kampeni ya mapema kabla ya Uchaguzi mkuu wa 2027.

Akizungumza jijini Nairobi, Ethekon alisema Tume ya IEBC ina nia ya kufafanua mda wa kampeni na kuangazia masuala kuhusu utayarishaji wa uchaguzi kabla ya wakati.

“Nchini Kenya, kila siku, kila saa inafanana na msimu wa kampeni. Iwapo mtu atahudhuria hafla ya mazishi anazungumzia uchaguzi, hivyo inamaanisha ni kampeni? aliuliza Ethekon.

Mwenyekiti huyo mpya wa IEBC alisema ni vigumu kuangazia mda mwafaka wa kampeni ya uchaguzi unapofaa kuanza.

Kuhusu suala la uchaguzi ndogo nchini, Ethekon alihakikishia wakenya kwamba ratiba kamili itatolewa mara tu michakato ya ndani ya tume hiyo itakapokamilika.

 “Kuhusu suala la muda wa uchaguzi mdogo, tutakuwa tukitangaza ratiba mara baada ya kamati ya uendeshaji kutoa taarifa zote kisha tutawasilisha maelezo. Kuweni na subira tutashughulikia ratiba,” alisema Mwenyekiti huyo.

Vile vile alikiri changamoto za kiutendaji zinazokabili tume hiyo japo akahakikishia wakenya kuwa hatua zinachukuliwa ili kuzitatua.

“Kulikuwa na baadhi ya mambo ambayo tuko nje ya udhibiti wetu, lakini tunafanya kazi usiku kucha kutekeleza shughuli hizi zote kama wale ambao wamepewa jukumu la kusimamia uchaguzi,” aliongeza Ethekon.

Hapo awali, Ethekon alisema uchaguzi mkuu wa 2027 utakuwa huru na wa haki, na kuondoa uwezekano wa wizi wa kura.

Taarifa ya Joseph Jira

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version