News
IEBC kuandaa chaguzi ndogo 23 nchini
Tume ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC inatarajiwa kuandaa chaguzi ndogo 23 zinazojumuisha viti sita vya bunge la kitaifa, kiti kimoja cha seneti, na nyadhifa kumi na sita za uwakilishi wadi.
Nafasi hizi zilijitokeza kutokana na sababu nyingi zikiwemo viongozi kufariki, wengine kuteuliwa katika majukumu mengine.
Miongoni mwa waliokuwa wabunge mashuhuri ambao kwa sasa viti vyao viko wazi ni pamoja na aliyekuwa seneta wa Baringo William Cheptumo, aliyekuwa mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi ambaye aliyeteuliwa kuwa waziri, na aliyekuwa mbunge wa Mbere Kaskazini Geoffrey Ruku, ambaye pia aliteuliwa katika baraza la mawaziri.
Kwengine ambako chaguzi ndogo zitaandaliwa ni pamoja na eneo bunge la Kasipul la mbunge Ong’ondo Were, eneo bunge la Banisa la Hassan Maalim pamoja na eneo bunge la Malava la Malulu Injendi ambao wote waliaga dunia.
Zaidi ya hayo, Mahakama ya rufaa iliridhia kufutwa kwa uchaguzi wa Harrison Kombe wa eneo bunge la Magarini kaunti ya Kilifi, na hivyo kuchangia katika orodha ya uchaguzi mdogo unaosubiriwa.
Hali hii inalazimu mchakato wa uchaguzi wa kujaza nafasi hizi zilizoachwa wazi na kuhakikisha uwakilishi unaendelea katika maeneo bunge husika.
Taarifa ya Joseph Jira