News
Gachagua amtaka Rais Ruto kuangazia usalama wa Mandera
Kinara wa chama cha DCP Rigathi Gachagua amekosoa serikali kwa kusalia kimya kuhusiana na madai ya uwepo wa jeshi la Jubaland hapa nchini.
Naibu huyo wa rais wa zamani sasa anamtaka rais William Ruto kutoa amri ya kufurusha jeshi hilo kutoka eneo la Mandera na kurejesha hali ya usalama.
Akizungumza katika ibada ya jumapili katika kanisa la PCEA Ongata Rongai, Agosti 31, 2025, Gachagua alikashifu uvamizi huo akisema uwepo wa jeshi hilo utasambaratisha usalama mjini humo.
Vile vile alimlaumu rais Ruto akisema anachukua mda kukabiliana na ufisadi nchini suala ambalo linaendelea kurejesha nyuma maendeleo ya taifa.
“Nakusema wabunge wote kazi yao ni kuchukua hongo na hatakubali hiyo maneno, nikafurahi sana kama ameamua hivyo kwa sababu yeye mwenyewe ndiye mwenye kuhonga wabunge, nilifikiri hayo maneno ya hongo yamefika mwisho lakini sasa yameongezeka, pale ikulu ndio mahali kwa hongo na ufisadi”,alidai Gachagua
Wakati huo huo waziri wa usalama wa zamani Fred Matiang’i aliyeandamana na Gachagua aliomba wakenya kuwaunga mkono wanaoendeleza kamapeni za kumuondoa rais William Ruto mamlakani.
Taarifa ya Joseph Jira