News
FIDA yakemea unyanyasaji wa kimtandao kwa wanawake
Shirika la wanawake mawakili nchini (FIDA) limekemea vikali ongezeko la visa vya dhulma za wanawake kwenye mitandao ya kijamii.
Mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo Anne Ireri alidai ripoti nyingi zilizotolewa tangu mwaka 2022 zilionyesha kuwa wanawake wengi wamepitia dhulma za kimtandao.
Akizungumza wakati wa kuadhimisha miaka 40 ya shirika hilo katika eneo la Diani kaunti ya Kwale, Ireri aliitaka serikali ya kitaifa kuhakikisha haki za wanawake zinalindwa kupitia uundaji wa sheria dhabiti.
“Fida imetoa ripoti nyingi sana kuhusu unyanyasaji wa kimtandao ukiangalia ile ripoti yetu ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2022, na zaidi ya hapo tumekuwa mstarti wa mbele kuhimiza haswa serikali kuu kupitia waziri wa maswala ya mawasiliano na jinsia, tuwe na sheria dhabiti ili vile ambavyo tumesikia ukiwa na shida na mimi usiende mtandaoni kunivua nguo, kuna njia ya kuweza kufuata haki zako”, alisema Ireri.
Ni kauli iliyoungwa mkono na gavana wa Kaunti hiyo Fatuma Achani aliyewataka watumizi wa mitandao kuzingatia sheria zilizowekwa na serikali.
Vil;e vile gavana Achani aliwaonya wakaazi wa Kwale dhidi ya kutumia vibaya mtandao na kuwasilisha malalamishi yao kwa taasisi za uchunguzi.
“Hii ukiipendelea itakuja pia kudhuru familia yako, naona ni kitu ambacho tunafaa kukisimamisha, kama uko na malalamishi ofisi yangu iko wazi, mtu ambaye anamalalamishi anafaa kufika ofisini ili tunatatua hilo tatizo”,alisema gavana Achani.
Taarifa ya Mwanahabari