National News
Chibule: Visa vya Dhulma za Kijinsi Vimepungua Kilifi
Serikali ya kaunti ya Kilifi imesema visa vya dhulma za kijinsia katika kaunti hiyo vimepungua kwa kiwango kikubwa.
Kulingana na Naibu Gavana wa kaunti hiyo Flora Mbetsa Chibule, visa hivyo viliongezeka zaidi msimu wa maambukizi ya virusi vya Corona, ambapo kaunti ya Kilifi iliorodheswa nafasi ya tatu nchini baada ya kaunti ya Bungoma na Samburu.
Chibule amesema kwa sasa ni asilimia 12.3 pekee ya visa hivyo vilivyoripotiwa tofauti na asilimia 30 wakati wa maambukizi ya Corona, akisisitiza kwamba juhudi hizo zimefanikiwa kupitia ushirikiano wa jamii na wadau mbalimbali.
Kiongozi huyo amedokeza kwamba serikali ya kaunti imetoa mafunzo kwa maafisa wa kutoa ushauri nasaha ili kusaidia kupambana na visa hivyo mashinani, akisema juhudi hizo zitaendelezwa sawa na kudhibiti madhila hayo.
Wakati uo huo ameweka wazi kwamba kaunti hiyo imekamilisha ujenzi wa sehemu salama ya kuwahifadhi watoto wanaopitia dhulma za kijinsia wakati kesi zao zikiendelea Mahakamani.