International News
Chanjo dhidi ya kisonono kutolewa karibuni
Chanjo za maradhi ya kisonono zitapatikana kwa wingi kuanzia Agosti 11, 2025 katika kliniki za afya Uingereza, katika jitihada za kukabiliana na viwango vya kuvunja rekodi vya maambukizi.
Awamu ya kwanza ya chanjo hizo itatolewa kwa wale walio katika hatari zaidi – wengi wao wakiwa wapenzi wa jinsia moja na wanaume wa jinsia mbili ambao wana historia ya wapenzi wengi wa ngono au magonjwa ya zinaa.
Huduma ya kitaifa ya afya Uingereza (NHS) ilisema hatua ya kusambaza chanzo hizo ni ya kwanza duniani, na inatabiriwa kuwa inaweza kuzuia visa vingi kama 100,000, na kunauwezekano wa NHS kuokoa karibu pauni milioni 8 katika muongo ujao.
Terrence Higgins Trust, ambao walifanya kampeni ya chanjo hiyo kuanzishwa nchini Uingereza, waliambia shirika la habari la BBC kuwa ni “ushindi mkubwa” kwa afya ya kijamii.
Kisonono ni maambukizi ya bakteria ambayo hupitishwa kupitia ngono isiyo salama.
Dalili zinaweza kujumuisha maumivu, kutokwa kwa maji yasiyo ya kawaida, kuvimba kwa sehemu za siri na utasa, lakini katika hali zingine kunaweza kuwa hakuna dalili kabisa.
NHS inasema inaweza kuepukwa kwa matumizi sahihi ya mipira ya kinga na kwa kukubali chanjo kama itatolewa.
Taarifa ya Joseph Jira