Sports
Carlos Alcaraz asonga raundi ya tatu US Open kwa ushindi wa kasi, Djokovic aponea chupuchupu
Mchezaji wa Tenisi Carlos Alcaraz raia wa Uhispania alitinga raundi ya tatu ya US Open hapo jana baada ya kushinda kwa seti tatu mfululizo kwa kishindo, huku Novak Djokovic akitoka nyuma kufanikisha ushindi baada ya kuonyeshwa kivumbi mapema.
Alcaraz, ambaye anaweza kukutana na Djokovic katika nusu-fainali endapo upangaji wa mechi hizo utafuatwa huko Flushing Meadows, alimfagia Muitaliano Mattia Bellucci 6-1, 6-0, 6-3 katika muda wa saa moja na dakika 36 pekee kwenye uwanja mkuu wa Arthur Ashe Stadium.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22, akiwa mchezaji namba mbili kwa ubora duniani, alitoa mikwaju ya kushambulia 32 katika mchezo wa kutawala dhidi ya Bellucci anayeridhiwa nafasi ya 65 duniani, ambaye mafanikio yake makubwa zaidi katika Grand Slam yalikuwa kufika raundi ya tatu Wimbledon mapema mwaka huu.
“Kwa kweli nimecheza vizuri sana, kuanzia mwanzo hadi mpira wa mwisho,” alisema Alcaraz, ambaye sasa atakutana na Muitaliano mwingine, Luciano Darderi (mbegu ya 32) katika raundi inayofuata.
“Kadri ninavyotumia muda mchache uwanjani ndivyo ilivyo bora zaidi kwangu, nipate kulala mapema,” aliongeza.
Wakati huohuo Jumatano, gwiji kutoka Serbia, Novak Djokovic, alihifadhi ndoto yake ya kunyakua taji la kihistoria la Grand Slam la 25 baada ya kumbwaga Mmarekani aliyeingia kwa kufuzu, Zachary Svajda, kwa seti nne.
Djokovic, hata hivyo, alilazimika kupambana baada ya kupoteza seti ya kwanza kabla ya kutwaa ushindi wa 6-7 (5/7), 6-3, 6-3, 6-1.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 38 alisema ingawa hayupo katika kiwango chake cha juu kwa sasa, anatumai kupata mwendelezo bora kadri mashindano yanavyoendelea.
“Ndio ninachotarajia, kadri ninavyosonga mbele kwenye mashindano ndivyo ninavyohisi vizuri zaidi kuhusu mchezo wangu,” alisema.
Ushindi huo unamweka Djokovic katika raundi ya tatu ya US Open kwa mara ya 19, akilingana na rekodi ya kihistoria, ambapo atakutana na Muingereza Cameron Norrie, aliyembwaga M-Argentina Francisco Comesana 7-6 (7/5), 6-3, 6-7 (0/7), 7-6 (7/4).
Katika mechi nyingine za wanaume Jumatano, Mnorwe Casper Ruud (mbegu ya 12) na finalisti wa US Open 2022, aliondoshwa na Mbelgiji Raphael Collignon baada ya kupoteza 6-4, 3-6, 3-6, 6-4, 7-5.
Mchezaji wa Marekani Taylor Fritz (mbegu ya 4) aliendelea salama kwa kumbwaga M-South Africa Lloyd Harris 4-6, 7-6 (7/3), 6-2, 6-4, huku rodha ya Marekani ikiimarishwa na Frances Tiafoe (mbegu ya 17), aliyemshinda mchezaji wa kufuzu Martin Damm kwa seti nne, 6-4, 7-5, 6-7 (8/10), 7-5.