Sports
Calafiori Aipa Arsenal Ushindi Dhidi ya Man United; Chelsea Wakwama Kwa Sare Tasa na Palace
Safari ya Arsenal kutafuta ubingwa wa Ligi Kuu ya EPL ilianza kwa ushindi muhimu baada ya bao la Riccardo Calafiori kuipa ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Manchester United, Jumapili. Wakati huo huo, mabingwa wa dunia Chelsea walinusurika kwa sare tasa ya 0-0 dhidi ya Crystal Palace ugani Darajani.
Baada ya kumaliza katika nafasi ya pili kwa misimu mitatu mfululizo, presha iko kwa kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, kuhakikisha analeta taji la kwanza la ligi kwa klabu hiyo tangu msimu wa 2003/04.
Ingawa hawakuwa wa kuvutia sana uwanjani Old Trafford, Arsenal walijinyakulia alama tatu muhimu kufuatia kosa kubwa la kipa wa muda wa United, Altay Bayindir. Mlinda lango huyo wa kimataifa wa Uturuki alishindwa kudaka kona ya Declan Rice dakika ya 13 na kumwachia Calafiori nafasi rahisi ya kufunga kwa kichwa.
“Matokeo makubwa,” alisema Arteta. “Mchezo wa kwanza wa msimu, na ukiwa Old Trafford ambapo unahisi wanajaribu kujenga kitu.”
United waliwapa nafasi ya kwanza washambuliaji wapya waliogharimu pauni milioni 200 — Matheus Cunha, Bryan Mbeumo na Benjamin Sesko — lakini walishindwa kupenya ukuta wa ulinzi wa Arsenal ambao ndio bora zaidi kwa misimu miwili iliyopita.
Patrick Dorgu alipiga shuti kali lililogonga mwamba na kukaribia kuisawazishia United, huku kipa wa Arsenal, David Raya, pia akifanya kazi kubwa kuzuia juhudi za Cunha na Mbeumo.
“Tumethibitisha leo kuwa tunaweza kushinda mechi yoyote ya EPL dhidi ya timu kubwa kama Arsenal,” alisema kocha wa United, Ruben Amorim. “Tulistahili matokeo tofauti, lakini tunapaswa kuangalia mbele kwa mchezo unaofuata.”
Kizungumkuti cha Chelsea;
Chelsea walionekana bado kuchoka baada ya mafanikio ya Klabu Bingwa Dunia huku wakikwamishwa na washindi wa Kombe la FA, Crystal Palace. Bao la mapema la Palace kupitia mpira wa adhabu wa Eberechi Eze lilikataliwa na VAR kwa madai kuwa Marc Guehi aliizuia ngome ya Chelsea.
Licha ya uvumi kwamba wanatazamiwa kujiunga na Liverpool na Tottenham mtawalia, nyota wa Palace, Guehi na Eze, bado walianza mchezo huo.