Sports

Boniface Muchiri Apandishwa Cheo KDF Baada ya Kung’ara CHAN 2024

Published

on

Winga wa Harambee Stars na Ulinzi Stars, Boniface Muchiri, amepandishwa cheo kwa heshima kutoka Sajenti wa Kawaida hadi Koplo katika Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF), hatua inayotambua mchango wake mkubwa kwa klabu yake na pia timu ya taifa.

Jenerali Charles Kahariri, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), ndiye aliongoza hafla ya kumpandisha cheo nahodha huyo wa Ulinzi Stars hapo jana, baada ya kuonyesha kiwango cha juu katika Mashindano ya Mataifa ya Afrika (CHAN) yanayoendelea.

Katika hotuba yake, Jenerali Kahariri alimpongeza Koplo Muchiri kwa nidhamu yake ya kipekee, kujituma na umahiri aliouonyesha katika ulingo wa kitaifa na kimataifa.
“Tunashukuru sana kwa kujitolea kwako, bidii na uchezaji bora ukiiwakilisha Kenya na vilevile KDF. Tunakutakia mafanikio katika majukumu yajayo na tuna imani utaendelea kung’ara,” alisema CDF.

Haya yanajiri baada ya nahodha wa Stars, Abud Omar, kumsihi Rais William Ruto aidhinishe kupandishwa cheo kwa mwenzake. Omar, ambaye amekuwa mstari wa mbele kusisitiza uongozi na huduma ya Muchiri, alichangia pakubwa kuhakikisha juhudi zake zinatambuliwa.

Muchiri mwenye umri wa miaka 29 alikuwa mchezaji muhimu katika safari ya Harambee Stars kufika robo-fainali ya CHAN 2024, ambapo alitoa pasi mbili muhimu za mabao kabla ya Kenya kutolewa na Madagascar.

Shauku, kujituma na moyo wa kupambana aliouonyesha uwanjani si tu umelifufua taifa, bali pia umewatia moyo wachezaji wachanga wengi.

Amezaliwa na kulelewa na mama mmoja huko Nambale, Kaunti ya Busia, safari ya Muchiri inaakisi ustahimilivu na uvumilivu.

Vipaji vyake vilianza kung’aa katika klabu ya Amagoro FC, timu ya mitaani iliyowahi kutoa wachezaji nyota wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL).

Wakati akiwa Shule ya Upili ya St. Mary’s Kibabii Boys, mwalimu mkuu Peter Lunani aligundua kipaji chake na kumlea hadi akavunja kuta za soka la kulipwa.

Baada ya kuhitimu kidato cha nne na alama ya C+, Muchiri alisaini mkataba wake wa kwanza na Nzoia Sugar, kisha kujiunga na Sony Sugar FC na baadaye Tusker FC, ambapo chini ya kocha Robert Matano, alinyanyua kombe la Ligi Kuu ya Kenya pamoja na kombe la Shield Cup.

Karieryake pia ilimfikisha Marekani alipojiunga na klabu ya Los Angeles Force kwa muda wa miezi sita kwenye National Independent Soccer Association, kabla ya kurejea nyumbani na kung’aa na Ulinzi Stars.

Katika kikosi cha kijeshi, Muchiri ameweka rekodi ya kuvutia akiwa mfungaji bora wa timu kwa misimu mitatu mfululizo, na hivyo kuimarisha zaidi urithi wake.

Leo, kupandishwa kwake cheo ndani ya KDF ni ushahidi wa umahiri wake maradufu – katika michezo na pia kwenye huduma ya kijeshi.

Kutoka viwanja vya vumbi vya Busia hadi kuivaa jezi ya Stars na beji ya KDF kwa fahari, simulizi ya Boniface Muchiri ni ya ustahimilivu, nidhamu na uzalendo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version