National News
Mahakama Kuu Yamtupa Nje Gavana Mwangaza
MAHAKAMANI – Gavana wa Meru Kawira Mwangaza amepata pigo baada ya Mahakama kuu kuidhinisha uamuzi wa bunge la Seneti la kumtimua Mamlakani.
Uamuzi huo imejiri baada ya bunge la Seneti kupiga kura kwa kauli moja na kuidhinisha malalamishi yaliowasilishwa na bunge la kaunti ya Meru dhidi ya kiongozi hiyo.
Malalamishi hayo dhidi ya Gavana Mwangaza ni pamoja na ukiukaji wa katiba, utumizi mbaya wa ofisi ya umma, ubadhirifu wa fedha miongoni mwa mashtaka mengine.
Akitoa uamuzi huo, Jaji wa Mahakama kuu Bahati Mwamuye, amesema Mahakama imeona kwamba ombi lililowasilishwa na Gavana Mwangaza la kupinga uamuzi wa bunge la Seneti halina uzito wowote na Mahakama ikatupilia mbali ombi hilo la Mwangaza.
“Mahakama hii imeona kwamba ombi lililowasilishwa na Gavana Mwangaza halina uhalali na kutulipiwa mbali. Notisi ya Gazeti la serikali iliyochapishwa tarehe 21 Agosti 2024 ya kumwondoa afisini imethibitishwa”, Jaji Mwamuye.
Mahakama imeamua kwamba bunge la Seneti halikukiuka maagizo yoyote ya Mahakama licha ya Gavana Mwangaza kulalamika kwamba bunge hilo liliegemea upande mmoja na kwamba Mahakama haikupata uthibitisho wowote juu ya madai hao.
Mahakama hata hivyo haikupata ushahidi wowote kwamba alinyimwa nafasi ya kuzungumza na ilibainisha kwamba timu yake ya mawakili haikuleta pingamizi lolote kuhusu muda uliotengwa kwa ajili ya utetezi wake.
Naibu Gavana wa kaunti hiyo ya Meru Isaac Mutuma M’Ethingia huenda akaapishwa rasmi na kuchukua nafasi ya Gavana katika kaunti hiyo ili kuhakikisha shughuli mbalimbali za kaunti zinaendelea vyema, iwapo Mwangaza hatakata rufaa kuhusu uamuzi huo wa Mahakama kuu.