Entertainment
Diamond Amshtaki Ex Wake Kwa Kutumia Picha Za Zamani Kum’blackmail
Mmiliki na mjasiriamali wa lebo ya Wasafi Media na WCB Wasafi, Diamond Platnumz ameelekea mahakamani kumshtaki mpenzi wake wa zamani kwa kile alisema kwamba anatumia picha za zamani wakiwa pamoja kumchafulia jina.
Akithibitisha hatua hiyo kupitia ukurasa wake wa Instagram, Diamond alisema kwamba mwanamke huyo ambaye hakuweka wazi utambulisho wake amekuwa akimchafulia jina kwa kutumia video za zamani wakiwa pamoja.
Msanii huyo alithibitisha kwamba ameona baadhi ya video hizo zikisambazwa na mpenzi wake wa zamani mitandaoni kwa lengo la kumharibia jina licha ya kuachana muda mrefu uliopita.
“Nimeona kuna clip zinasambazwa mtandaoni zinazonihusu…clip hizo ni za zamani, mwaka 2023, na zina zaidi ya miaka miwili nyuma…na mwanamke huyo pia niliachana nae takriban miaka miwili sasa,” Diamond alisema.
Msanii huyo alieleza kwamba video hizo zinalenga kumharibia hata penzi lake la sasa na Zuchu, akiweka wazi kwamba alishamjulisha mpenzi wa sasa kuhusu kumalizika kwa penzi hilo la zamani.
“Lakini pia nilimueleza mwenzangu niliye nae na tukasameheana na kuanza maisha mapya…” alisema.
Baada ya kugundua kwamba lengo la mwanamke huyo kutumia video hizo za zamani wakiwa pamoja ni kumharibia, Diamond alisema tayari amelikabidhi mikononi mwa idara husika kisheria.
“Mwanamke huyo sasa ameamua kutumia clip hizo na kuambatanisha na jumbe za uongo kwa lengo la kuni blackmail na kutengeneza fedha, jambo hili lishafikishwa katika mamlaka husika na taratibu za kisheria zinafuatwa. Shukran,” alisema.