News
Vijana 9 Wametiwa Nguvuni na Polisi Msambweni
Idara ya usalama kaunti ya Kwale imefanikiwa kuwatia nguvuni washukiwa 9 wa uhalifu wanaoaminika kuwa vijana wa vipanga katika eneo la Diani kaunti ya Kwale.
Kulingana na Kamanda wa Polisi eneo la Msambweni Robinson Lang’at, tisa hao walikuwa wamejihami kwa silaha hatari ikiwemo mapanga 11, visu 4, simu 5 za rununu na Mihadarati aina ya Bangi miongoni mwa vifaa vingine.
Lang’at amesema tangu idara ya usalama ianze oparesheni ya kiusalama katika eneo hilo wamefaulu kuwatia nguvuni vijana 145 wanaoaminika kuwa wahalifu na ambao wamekuwa wakitatiza usalama wa jamii.
Wakati huo huo amewataka wazazi kuchunguza mienendo ya watoto wao msimu huu wa likizo huku akiwahakikishia wakaazi wa eneo la Msambweni pamoja na wageni wanaolenga kuzuru eneo hilo kwamba usalama umeimarishwa.