Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC, imefichua kwamba inakabiliwa na upungufu wa fedha wa takriban shilingi bilioni 22.
Mwenyekiti wa IEBC, Erastus Ethekon, alisema changamoto za kifedha, pamoja na vikwazo vya kisheria na kiutendaji, zinaweka hatarini uwezo wa tume hiyo kuendesha uchaguzi huru, haki na uwazi.
Katika kikao na Wanahabari, Ethekon alisema upungufu huo umetokana na mahitaji mbalimbali ya kiutendaji, ikiwemo ununuzi wa vifaa vya uchaguzi, elimu ya mpiga kura, uajiri na mafunzo ya maafisa wa vituo vya kupigia kura, pamoja na kuboresha mifumo ya kiteknolojia.
Mwenyekiti huyo wa IEBC alisema tayari Tume hiyo imeanza mazungumzo na Hazina ya kitaifa, na itawasilisha rasmi ombi la ufadhili katika wiki zijazo, kwani inahitaji kima cha shilingi bilioni 63 japo tayari imepokea shilingi bilioni 41.
Akigusia suala la mipaka, Mwenyekiti wa IEBC alisema uwekaji mipaka unasalia kuwa msingi wa kikatiba, akisema kwamba tume hiyo imezidi muda unaohitajika wa kutathmini upya mipaka kwa miaka minane na 12.
Wakati huo huo alibainisha kwamba ukaguzi wa mwisho ulipaswa kukamilika ifikapo mwaka wa 2024 lakini hadi sasa suala hilo bado halijatekelezwa, akitaja kutokuwepo kwa muda mrefu kwa makamishna.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
