Naibu Chifu wa eneo la Sabaki eneo bunge la Magarini kaunti ya Kilifi Rachael Malingi amewahimiza kina mama wajawazito kuhakikisha wanafika hospitalini ili kujifungua salama.
Akizungumza mjini Malindi, Malingi alisema baadhi ya kina mama ambao ni wajawazito wanaenda kwa waombezi na wakunga badala ya hospitalini hali ambayo inahatarisha maisha ya mama na mtoto aliye tumboni.
Malingi alisema vifo vya kina mama kufariki wanapojifungua nyumbani vitadhibitiwa ikiwa watatilia maanani suala la kuenda hospitalini.
‘’Ningependa kuhimiza wale wazazi ambao bado wanapata watoto tafadhalini tukaweze kupata watoto hospitalini. Hii mambo ya kuenda kwa waombezi, mambo ya kuenda kwa waganga na wewe ni mjamzito hiyo hatutaruhusu’’ alisema Malingi.
Naye Teresiah Ilobi ambaye ni mhudumu wa afya kutoka shirika la Shamiri Afrika aliwahimiza wanaume kuambatana na wenza wao wajawazito hadi kliniki ili kupata ushauri wa kitaalamu kuhusu afya ya uzazi.
‘’ Wababa muambatane na wamama kuelekea hospitalini ina umuhimu wake.Sisi kama wahudumu wa afya tunapata wakati mgumu sana wakati mama amefika na hali ya afya yake haijui’’ alisisitiza Ilobi
Ni kauli ambayo iliungwa mkono na Malingi na kusisitiza umuhimu wa wananchi kuwa na hulka ya kufika hospitalini kufanyiwa vipimo vya afya mara kwa mara.
Katika suala la usafi Malingi alisema mji wa Malindi unapaswa kusafishwa ili kudhibiti mlipuko wa magonjwa mbalimbali huku baadhi ya wakazi wakiinyooshea kidole cha lawama ofisi husika.
Taarifa ya Janet Mumbi
