Rais Ruto: Usajili wa makurutu wa NYS utaongezeka hadi laki moja

Rais Ruto: Usajili wa makurutu wa NYS utaongezeka hadi laki moja

Rais William Samoei Ruto amesema usajili wa makurutu watakaojiunga na huduma ya vijana kwa taifa NYS utaongezeka kutoka vijana 18,000 hadi 100,000 katika miaka mitatu ijayo.

Akizungumza katika hafla ya 89 ya kufuzu kwa makurutu wa NYS katika kambi ya Gilgil katika kaunti ya Nakuru, Rais Ruto alisema ongezeko hilo linaonyesha uimarishaji katika mafunzo na ujuzi ili kudhibiti hali ya ukosefu wa kazi miongoni mwa vijana nchini.

‘’Serikali pia imeanzisha mipango kadhaa inayolenga kukabiliana na ukosefu wa ajira kwa vijana’’ alisema rais Ruto.

Rais Ruto pia alisema NYS imekuwa yenye tija katika masuala ya kama ya kilimo, uhandisi na ujenzi miongoni mwa mengine.

Makurutu wa NYS katika kambi ya Gilgil katika kaunti ya Nakuru

“Tayari inazalisha unga wa mahindi, mafuta ya kupika, na bidhaa za matunda, kupunguza gharama, na kuzalisha mapato. Hivi karibuni, NYS pia itatoa sifa zinazotambulika kitaifa na kimataifa.” aliongeza rais Ruto.

Zaidi ya makurutu 18,000 idadi ambayo ni kubwa zaidi katika historia ya NYS, baada ya kufanya mafunzo ya miezi sita rais Ruto aliagiza wizara ya mambo ya ndani kuhakikisha makurutu 4000 wanajiunga na huduma ya kitaifa kwa polisi wakati wa kuwasajili makurutu 10,000 katika usajili ujao wa maafisa wa polisi.

Waliohudhuria hafla hiyo ni Gavana wa Nakuru Susan Kihika, waziri wa utumishi wa umma nchini Geoffrey Ruku na Kamanda Mkuu wa NYS James Tembur.

Taarifa ya Janet Mumbi