News
Tungule: Umaskini ndio changamoto ya elimu Ganze
Mbunge wa Ganze kaunti ya Kilifi Kenneth Tungule amesema wanafunzi wengi katika eneo bunge hilo hawafanyi vyema masomoni kutokana na hali ya umasikini na njaa.
Tungule alisema licha ya kuwa baadhi ya wanafunzi ni werevu imekuwa vigumu kwao kupata alama nzuri shuleni kwani wengi wao wanatoka kwenye familia ambazo hazina uwezo hasa za kifedha.
Tungule alitoa wito kwa serikali kuu kuweka mikakati ifaayo ya namna itaimarisha eneo hilo kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo ili kudhibiti hali ya umasikini.
Tungule alisema ikiwa umasikini utadhibitiwa wanafunzi katika eneo hilo wataenda shuleni bila changamoto zozote na hata viwango vya elimu vitaimarika.
“Hawa wanafunzi wa Ganze ninavyowajua mimi kwasababu pia mimi nimesomea shule za Ganze, sisi akili zetu ziko sawa, watoto wa Ganze ni werevu sana lakini kitu ambacho kinawatatiza ni umasikini ndani ya nyumba zao’’, alisema Tungule.
Vilevile, Tungule alisema mradi wa umeme ambao unaendelezwa na serikali kuu katika eneo hilo, utawafaidi wenyeji katika kuendeleza shughuli zao mbalimbali zikiwemo za biashara na uchumi wa eneo la Ganze unatarajiwa kuimarika pia kwa asilimia kubwa.
“Kuna watu zaidi ya elfu mbili ambao tanawaunganishia umeme huo na hiyo yote tunafanya bure bila kulipa hata shilingi na gharama yote imelipwa na serikali kuu’’, aliongeza Tungule
Taarifa ya Janet Mumbi