Rwanda yatangaza udhamini wa muda mrefu na Los Angeles Rams na LA Clippers, na kuwa taifa la kwanza barani Afrika kushirikiana na NFL na NBA kwa ajili ya utalii.
Nembo ya utalii Visit Rwanda, inayoendeshwa na Bodi ya Maendeleo ya Rwanda (RDB), itaonekana kama mdhamini rasmi wa kiraka cha jezi cha LA Clippers, huku uwanja wa nyumbani wa Los Angeles Rams pia ukibeba chapa hiyo.
“Ushirikiano huu unatuwezesha kupeleka uzuri wa kipekee wa asili ya Rwanda na bioanuwai yake ya ajabu kwa watu wa Los Angeles pamoja na mashabiki wa NBA na NFL kote duniani,” alisema Jean-Guy Afrika, Mkurugenzi Mkuu wa RDB katika taarifa yake.
Nchi hiyo ya Afrika Mashariki imekuwa ikijitangaza kwa muda mrefu kama kitovu cha matukio makubwa ya michezo na kinara wa utalii wa ikolojia — ikiwa ni sehemu ya jitihada zake kuvutia wawekezaji na kuondoka kwenye kivuli cha mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.
Mnamo 2018, Rwanda ilikua mdhamini rasmi wa klabu ya soka ya Uingereza, Arsenal FC, ambapo nembo ya “Visit Rwanda” iliwekwa kwenye mikono ya jezi za wachezaji.
Kigali pia imeingia mikataba na vilabu vingine vya mpira wa miguu kama Paris Saint-Germain (PSG) na kwa sasa inapigania kuwa mwenyeji wa mashindano ya Formula One.
Wiki iliyopita, Rwanda pia iliandika historia kwa kuwa taifa la kwanza barani Afrika kuandaa mashindano ya dunia ya mbio za baiskeli, yaliyokamilika Jumapili.