Sports
Shabiki Apigwa Marufuku Viwanja Vyote Uingereza kwa Kumtusi Kibaguzi Antoine Semenyo
Mwanaume mmoja aliyekamatwa kwa tuhuma za kumtolea matusi ya kibaguzi mshambuliaji wa Bournemouth, Antoine Semenyo, wakati wa mechi ya ufunguzi ya Ligi Kuu ya Uingereza kwenye uwanja wa Anfield, amepigwa marufuku kuingia kwenye viwanja vyote vya mpira wa miguu nchini Uingereza.
Mchezo wa Bournemouth dhidi ya Liverpool siku ya Ijumaa ulisitishwa kwa muda dakika ya 29 baada ya Semenyo kumjulisha mwamuzi kuhusu tukio hilo.
Kwa mujibu wa Polisi wa Merseyside, mwanaume mwenye umri wa miaka 47 kutoka Liverpool alikamatwa Jumamosi kwa tuhuma za kosa la utovu wa nidhamu lenye misingi ya kibaguzi, na kwa sasa ameachiliwa kwa dhamana yenye masharti.
Masharti hayo ni pamoja na marufuku ya kuhudhuria mechi yoyote ya mpira wa miguu iliyoidhinishwa nchini Uingereza na kutoruhusiwa kwenda umbali wa ndani ya maili moja kutoka uwanja wowote ulioteuliwa wa mpira wa miguu.