News
Serikali yashinikizwa kukabili ajira za utotoni.
Maafisa wa idara inayoshughulikia maslahi ya watoto kaunti ya Kilifi wameshinikiza serikali kuu na zile za kaunti kuweka mikakati dhabiti ili kukabili suala la ajira za utotoni.
Wakiongozwa na Kevin Mugambi afisa wa idara ya watoto eneo la Kauma alitaja suala la umaskini kama chanzo kikuu cha watoto kushiriki aina hiyo ya ajira.
Akizungumza katika kipindi cha Coco asubuhi, Mugambi alisema raslimali zaidi zinafaa kuekezwa hasa katika mgao wa bajeti ya kitaifa utakaoelekezwa katika idara hiyo.
Kwa upande wake Omar Mohammed Afisa wa watoto eneo bunge la Ganze alionya wazazi kuepuka kuajiri watoto walio chini ya umri wa miaka 18, akisema watakabiliwa kisheria iwapo watapatikana.
“Kama wewe labda ni muajiri pahali popote ulipo na umeweza kuchukua mtoto ama mtu chini ya umri wa miaka 18 hiyo unaweza kushtakiwa, kwa hivyo kitu kizuri cha kufanya ni kwamba kama mtu hana kitambulisho cha kenya basi usimuajiri kwa sababu huyo ni mtoto na ikipatikana hiyo ni ajira ya utotoni”, Alisema Omar.
Taarifa ya Joseph Jira