Business
Serikali Yahimizwa Kuharakisha Leseni za Ndege Ili Kufanikisha Malengo ya Utalii 2027
Ili kufanikisha malengo ya taifa ya kupokea watalii milioni tano ifikapo mwaka 2027 serikali imehimizwa kuharakisha utoaji wa leseni kwa ndege na ndege za kukodi.
Wadau wa sekta ya utalii nchini wamesema leseni hizo zitasaidia katika kusafirisha watalii kutoka mataifa ya nje kuingia nchini.
Wakizungumza jijini Mombasa wakati wa kongamano la 21 la kila mwaka la chama cha wahudumu wa hoteli na wapishi (KAHC), Wakiongozwa na afisa mkuu Mtendaji wa chama hicho Mike Macharia, wameeleza kuwa ucheleweshaji wa utoaji wa leseni kwa mashirika mapya ya ndege umekuwa kikwazo kikubwa kwa ukuaji wa sekta hiyo.
Macharia aidha ameonya kuwa iwapo suala hilo halitashughulikiwa kwa haraka, basi taifa linaweza kupoteza fursa muhimu ya kukuza uchumi kupitia utalii.
Wadau hao pia wameitaka serikali kuweka mazingira ya kuwezesha uwekezaji zaidi katika sekta ya anga, hususan kwa mashirika yanayolenga kuleta watalii moja kwa moja kutoka masoko ya kimataifa.