Sports
Serikali Kuanzisha Maeneo Maalum ya Mashabiki Kutazama Mechi za CHAN Jijini Nairobi
Waziri wa Michezo, Salim Mvurya, amesema kuwa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) litaanzisha maeneo maalum ya mashabiki jijini Nairobi kwa ajili ya kutazama mechi za CHAN 2024, ikiwa ni hatua ya kupunguza msongamano katika Uwanja wa Kasarani wakati wa pambano la Harambee Stars dhidi ya Zambia.
Waziri Mvurya alitoa kauli hiyo mapema leo alipokuwa akiongoza kikao cha usalama kuhusu masuala ya mashabiki katika Uwanja wa Kasarani.
Hatua hii inafuatia masharti mapya yaliyowekwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) kwa Harambee Stars baada ya kutokea vurugu za mashabiki kwenye mechi iliyopita. CAF imeagiza mashabiki 27,000 pekee kuruhusiwa kuingia uwanjani Kasarani kwa mchuano wa Jumapili, la sivyo timu ya taifa inaweza kuwekewa masharti makali zaidi, ikiwemo kulazimishwa kucheza mechi zake za nyumbani nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Waziri Mvurya, mpango huu wa maeneo ya kutazamia mechi utasaidia mashabiki wengi ambao hawatapata tiketi kushuhudia mechi hiyo uwanjani, lakini watapata fursa ya kushabikia vijana wa nyumbani katika mazingira salama na rafiki.