News

Rais Ruto: Tumeweka mikakati kuimarisha maendeleo Pwani

Published

on

Rais William Ruto amesema wanaendeleza mikakati thabiti katika kuhakikisha kuna miradi mingi ya maendeleo ambayo inatekelezwa kaunti ya Kilifi na kanda ya Pwani kwa jumla.

Rais Ruto ambaye aliwahutubia waombolezaji katika hafla ya mazishi ya Gedion Baya Mung’aro ambaye ni babake gavana wa kaunti ya Kilifi, Gedion Maitha Mung’aro eneo Dabaso katika wadi ya Watamu, alisema shilingi bilioni 3 zimetengwa kufanikisha mradi wa umeme kutoka Malindi kupitia Weru hadi Kilifi.

Rais Ruto pia alisema zaidi ya nyumba elfu 20 zitaunganishwa na mradi wa umeme na pia shilingi bilioni mbili na laki mbili zimetolewa kuhakikisha hilo linafanikishwa.

“Ni jukumu la serikali kuu kuhakikisha kila eneo hapa nchini linatekelezewa miradi ya maendeleo bila kutengwa na pwani ni miongoni mwa maeneo hayo ambayo yanafaa kupata maendeleo’’ Alisema Rais Ruto

Wakati huo huo, Rais Ruto akizungumzia bima ya afya ya SHA, alisema hakuna mkenya ambaye atakosa kutibiwa hospitalini kutokana na ukosefu wa fedha na kuwashinikiza wenyeji wa kaunti ya Kilifi na Wakenya kwa jumla kujisajili kwenye bima hiyo ili watibiwe bila changamoto zozote.

“Tunasema matibabu ni haki ya kila mkenya sababu katiba ndio inasema hivyo’’ Alisema Rais Ruto.

Taarifa ya Janet Mumbi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version