News

Bi Rachel azindua mpango wa “lishe bora” shuleni

Published

on

Ofisi ya mke wa Rais Bi Rachel Ruto, imezindua mpango wa lishe bora kupitia utoaji wa maziwa kwa watoto wa shule kama sehemu ya mpango wa kuboresha afya na kuongeza nguvu kwa watoto ili waweze kuendelea na masomo yao shuleni bila changamoto zozote.

Akingumza katika Shule ya msingi ya Kachororoni eneo bunge la Ganze kaunti ya Kilifi, Bi Rachel alisema mpango huo wa Feed One End Hunger ambao umefanikishwa kwa ushirikiano na Bodi ya Maziwa nchini KDB na Muungano wa ushirika wa maziwa, Meru utadhibiti utapiamlo kwa watoto.

Bi Rachel Ruto alisema wanafunzi wengi nchini ambao wanatoka kwenye familia zisizojiweza hasa kifedha wamekuwa wakisitisha masomo yao kutokana na njaa na utapiamlo kutokana na ukosefu wa lishe bora.

“Afya ya mtoto ni muhimu sana na ikiwa mpango huu wa lishe bora utakumbatiwa, wanafunzi wengi shuleni watafanya vyema katika masomo yao”, alisema Bi Rachel Ruto.

Kwa upande wake Katibu mkuu katika Wizara ya Kilimo nchini Jonathan Mueke ambaye alikuwa ameandamana na Bi Rachel Ruto aliupongeza mpango huo akiutaja kama hatua muhimu ya kufanikisha elimu shuleni.

Naye Naibu Gavana wa kaunti ya Kilifi Flora Mbetsa Chibule alisema tangu kuzinduliwa kwa mpango wa lishe shuleni kaunti ya Kilifi, wanafunzi wengi wamekuwa wakijiunga na shule mbalimbali ikilinganishwa na miaka ya nyuma na kuahidi kushirikiana na ofisi ya mke wa rais Bi Rachel Ruto katika kuhakikisha unafikishwa vilivyo.

Hata hivyo Mbunge wa Ganze Kenneth Kazungu Tungule alitoa wito kwa Rais William Samoei Ruto kujenga barabara ya Kilifi – Ganze – Bamba ili kuimarisha shughuli za uchukuzi eneo hilo.

Kauli ambayo iliungwa mkono na Mwakilishi wa Kike kaunti ya Kilifi Getrude Mbeyu, ambaye alisema eneo bunge la Ganze lina raslimali nyingi na huenda Ganze ikawa eneo tajiri zaidi nchini iwapo raslimali hizo zitatumika ipasavyo na kuipongeza Serikali kuu kupitia Wizara ya Utalii na wanyamapori nchini kutoa kima cha shilingi milioni 60 za fidia kwa wakaazi wa kaunti ya Kilifi walioathiriwa na wanyamapori.

Taarifa ya Janet Mumbi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version