Sports
Police Bullets Kuanza kampeni ya CECAFA kwa matarajio ya kutwaa ubingwa
Mkufunzi wa kilabu ya Kenya Police Bullets, Beldine Odemba, amesema timu yake iko tayari kupambana hadi mwisho na kutwaa ubingwa wa CECAFA Qualifiers za Ligi ya Mabingwa wa Wanawake wa CAF.
Mabingwa wa FKF Women’s Premier League wataanza kampeni yao siku ya hapo kesho, Septemba 4, 2025, dhidi ya Kampala Queens ya Uganda katika Uwanja wa Nyayo National Stadium. Wapo Kundi A, ambalo pia linajumuisha Denden FC ya Eritrea.
Kundi B lina mabingwa watetezi Commercial Bank of Ethiopia (CBE), pamoja na Top Girls Academy ya Burundi na Rayon Sports WFC ya Rwanda.
Kundi C linaongozwa na JKT Queens ya Tanzania, wakijiunga na Yei Joint Stars ya Sudan Kusini na JKU Princess ya Zanzibar.
“Wasichana wako tayari kabisa kuanza mashindano ya CECAFA.wamepata mafunzo makali na naamini faida ya kucheza nyumbani itatufanikisha kutwaa taji na kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa wa Wanawake wa CAF. Kama nilivyosema awali, tutaheshimu kila timu na hatuwezi kuidharau timu yoyote,” alisema Odemba.
Mwalimu huyo akiwahimiza mashabiki kujitokeza kwa wingi katika viwanja vya Nyayo Stadium na Ulinzi Complex kuwashangilia Bullets.
Kwa Police Bullets, dhamira ni ya kulipiza kisasi.
Mwaka jana mjini Addis Ababa, walikaribia kufuzu lakini wakapoteza 1-0 dhidi ya CBE kwenye fainali. Safari hii, wamedhamiria kutumia nafasi yao ipasavyo wakiwa nyumbani.