News

Pigo kwa Spika Mwambire, apokonywa walinzi

Published

on

Karani wa bunge la kaunti ya Kilifi Emmanuel Ngala ameagiza kuondolewa kwa walinzi wanaolinda makaazi ya Spika wa bunge la kaunti hiyo Teddy Mwambire.

Kulingana na barua iliyoandikwa na Ngala kupitia bunge hilo na kuwasilishwa kwa Spika Mwambire, walinzi wote ambao wanalinda makaazi ya Spika huyo kupitia kampuni ya Ulinzi ya Ismax, hawatatekeleza tena majukumu yao.

Barua hiyo pia imefafanua kwamba hatua hiyo ni kutokana na bunge la kaunti ya Kilifi kumtimua Mamlakani Spika Mwambire Juni 30 mwaka huu baada ya Wawakilishi wadi 40 kati ya 51 kupiga kura ya kutokuwa na imani naye na kumbadua ofisini.

Barua hiyo hata hivyo imeweka wazi kwamba itamlazima Mwambire kutumia walinzi wa kibinafsi katika kufanikisha usalama wake na wala sio walinzi wanaotambulika na bodi ya bunge la kaunti ya Kilifi.

Haya yamejiri huku Spika Mwambire akipata idhini ya Mahakama kuu ya Malindi kuendelea na majukumu yake ya kikazi kufuatia kesi ambayo iliwasilishwa Mahakamani na wakenya wawili wanaopinga uamuzi wa bunge hilo wa kumtimua ofisini Spika Mwambire.

Taarifa ya Mwahoka Mtsumi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version