Sports
Ogam Aibeba Harambee Stars, Kenya Yatinga Robo Fainali kama Vinara wa Kundi ‘A’
Mshambuliaji nyota Ryan Wesley Ogam kwa mara nyingine tena aliibuka shujaa, akifunga bao katika mechi ya pili mfululizo na kuisaidia Harambee Stars kuibwaga Zambia’s Chipolopolo 1-0 katika uwanja wa Moi International Sports Centre, Kasarani, Jumapili alasiri, na kufuzu robo fainali wakiwa vinara wa Kundi ‘A’.
Bao la ushindi la Ogam — shuti maridadi kwa mguu wake wa kushoto akiwa ndani ya boksi — liliihakikishia Kenya nafasi ya kwanza kwa alama 10. Stars sasa watavaana na Madagascar kwenye robo fainali katika uwanja huo huo siku ya Ijumaa.
Wakati huohuo, Morocco waliilaza DR Congo 3-1 katika uwanja wa Nyayo National Stadium na kumaliza nafasi ya pili nyuma ya Kenya. Atlas Lions sasa watapambana na vinara wa Kundi ‘B’, Tanzania, jijini Dar es Salaam, pia siku ya Ijumaa.
DR.Congo ilimaliza ya tatu na alama sita huku Angola ikimaliza ya nne na alama nne nayo Zambia ikivuta mkia bila alama yoyote na kuaga mashindano hayo ya Chan.