News
Ofisi ya ODPP kufungua mashtaka ya mauaji dhidi ya Masinde
Mkurugenzi wa mashtaka ya umma, Renson Ingonga, ameidhinisha mashtaka ya mauaji dhidi ya afisa wa polisi Barasa Masinde.
Masinde anadaiwa kuhusika moja kwa moja na mauaji ya mchuuzi wa barakoa Boniface Kariuki aliyepigwa risasi katikati mwa jiji la Nairobi wakati wa maandamano ya kupinga mauaji ya Albert Ojwang.
Kwenye taarifa iliyotolewa Julai 10, 2025, Ingonga alisema ushahidi uliokusanywa unatosha kufungua kesi ya mauaji dhidi ya afisa huyo wa Polisi, akisisitiza kwamba ni lazima haki ipatikane kwa familia ya marehemu Boniface.
Afisa mwingine aliyekuwa anachunguzwa kwa kuhusika na tukio hilo, Duncan Kiprono, aliondolewa lawama na kuachiliwa huru kwa kukosa ushahidi wa moja kwa moja dhidi yake.
Familia ya marehemu Boniface pamoja na Wanaharakati wa haki za binadamu wamekuwa wakishinikiza haki itendeke, wakitaka wote waliohusika na mauaji ya Boniface wakabiliwe kisheria.
Afisa Masinde anatarajiwa kufikishwa Mahakamani siku zijazo kujibu mashtaka yanayomkabili, huku serikali ikishikilia kwamba maafisa wa polisi wanaokiuka majukumu yao ya kikazi ni lazima wawajibishwe.
Itakumbukwa kwamba Juni 17 mwaka huu wakati wa maandamano ya kupinga mauaji ya Mwanablogu na Mwalimu Albert Ojwang, vurugu zilishuhudiwa katikati mwa jiji la Nairobi na kusababisha baadhi ya vijana wa Gen Z kupoteza maisha yao akiwemo Boniface Kariuki.
Taarifa ya Elizabeth Mwende