Mahakama ya Kilifi imetoa hukumu kwa washtakiwa zaidi ya 10 waliowasilishwa Mahakamani wakikabiliwa na mashtaka mbalimbali ikiwemo kesi za unajisi na makosa ya jinai.
Katika vikao vya Mahakama siku ya Jumatano tarehe 3 June 2026, Hakimu Ivy Wasike ametoa hukumu hizo kwa watuhumiwa hao huku wengine wakifungwa kwa zaidi ya miaka 30 gerezani.
Simon Ngala, Aliwali Ali Mwalimu, Christopher Buru, miongoni mwa wengine zaidi ya 10 walifikishwa katika Mahakama ya Kilifi na kuhukumiwa kufuatia mashtaka mbalimbali yanayowakabili ikiwemo mashtaka ya unajisi na makosa ya jinai.
Hakimu wa Mahakama ya Kilifi Ivy Wasike, alimhukumu kifungo cha miaka 30 gerezani Simon Ngala baada ya kupatikana na hatia ya kumnajisi mtoto wa miaka 13 kisha akamtorosha kwao kwa kipindi cha mwezi mzima.
Mwengine ni Aliwali Ali Mwalimu, aliyehukumiwa kifungo cha miaka 25 kufuatia mashtaka ya kumpachika ujauzito mtoto wa miaka 13 licha ya kuomba msamaha Mahakamani.
Wakati wa kutoa hukumu hizo, Hakimu Wasike alisikitishwa na kukithiri kwa visa vya watoto kupotea na kisha kunajisiwa katika kaunti ya Kilifi.
Kiongozi wa mashtaka katika Mahakama hiyo Nancy Njeru alipinga vikali ombi lililowasilishwa Mahakama la kutaka washtakiwa wasamehewe, kwanin wengine walidai kwamba walishirika makosa hayo bila kukusudia, akisema hukumu hizo zitakuwa funzo kwa watu wenye hulka hizo katika jamii.
Mbali na hukumu za kesi za unajisi, Christopher Buru alihukumiwa kifungo cha miaka miwili gerezani akikabiliwa na mashtaka ya wizi baada ya kupatikana na hatia ya kutumia pesa za mlalamishi Saumu Nyevu aliyekuwa akimtumia pesa alipokuwa akifanya kazi katika milki za kiarabu, kosa lililomchukiza zaidi Hakimu Wasike.
Taarifa ya Teclar Yeri
