Polisi waonya wananchi dhidi ya mauaji ya wazee Kwale

Polisi waonya wananchi dhidi ya mauaji ya wazee Kwale

Idara ya usalama kaunti ya Kwale imewaonya wananchi dhidi ya kuchukua sheria mikono na kusababisha maafa katika jamii kwa kisingizio cha kuwaua wazee kwa tuhma za uchawi.

Kamishna wa kaunti hiyo David Rotich alisema maafisa wa usalama wameanzisha msako mkali dhidi ya wale waliohusika katika matukio matano ya mauaji ya wazee.

Akizungumza katika bustani ya Baraza mjini Kwale, Rotich alisema mauaji dhidi ya wazee yameripotiwa kuchipuka upya na kwamba hivi karibuni katika eneo la Lungalunga na Kinango kumeripotiwa visa vitano vya mauaji ya wazee.

“Nimetoa amri kwa kamati ya usalama eneo la Lungalunga na Kinango kuhakikisha wale wanaohusika wanakamatwa na kufikishwa Mahakamani, hatuwezi ruhusu visa hivyo kuendelea na wazee ni watu muhimu katika jamii’, alisema Rotich.

Kwa upande wake Naibu Gavana wa Kwale Chimera Kombo amepongeza ushirikiano unaoendelea kati ya serikali kuu na kaunti ya Kwale, akisema umechangia wakaazi wa kaunti hiyo kushuhudia maendelea, akitoa mfano wa barabara ya Kwale-Kinango.

Taarifa ya Mwanahabari wetu