Ukataji wa miti kaunti ya Kilifi wakashifiwa

Ukataji wa miti kaunti ya Kilifi wakashifiwa

Wadau mbalimbali wa mazingira katika kaunti ya Kilifi waliungana katika chuo kikuu cha pwani kuadhimisha siku ya mazingira ulimwenguni, hafla ambayo ilianza na zoezi la upanzi wa miche elfu 5.

Katika hafla ambayo iliongozwa na mkurugenzi wa mazingira kaunti ya Kilifi, Jimmy Yaa walisema licha ya taifa kuwekeza katika matumizi ya kawi safi na upanzi wa miche, bado juhudi zaidi zinapaswa kuwekwa kukabiliana na changamoto za kimazingira zinazotatiza harakati hizo.

Kwa upande wa Ruwa Kalama kutoka idara ya misitu kaunti ya Kilifi alisisitiza haja ya Wananchi kupanda miche ya matunda na kuwaonya wakaazi dhidi ya kukata miti kiholela ili kukabiliana na madailiko ya hali ya anga.

“Kadri tunavyopanda miche, tusisahau kupanda ile ya matunda na pia kaunti ya Kilifi ni Kati ya zile kaunti ambazo zinakata miti kihole”, alisema Kalama

Naye Kamanda wa Polisi eneo la Kilifi Kaskazini, kaunti ya Kilifi Stanley Tanui, alisema idara ya usalama imekuwa katika mstari wa mbele kuhakikisha sheria ambazo zinawekwa kudhibiti uchafuzi wa mazingira zinatekelezwa vilivyo.

“Kama idara ya usalama Kilifi Kaskazini, hata sisi tunahusika pakubwa katika uhifadhi wa mazingira na kuhakikisha sheria za kudhibiti uchafuzi wa mazingira zinatekelezwa vilivyo” alisema Tanui

Maadhimisho haya yalilenga kuhamasisha jamii kuchukua hatua madhubuti za kupunguza athari za uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya hali ya anga kote ulimwenguni.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa”

Taarifa ya Janet Mumbi