DCI waomba muda zaidi dhidi ya kesi ya Keziah

DCI waomba muda zaidi dhidi ya kesi ya Keziah

Mahakama ya Kilifi imeagiza kuendelea kuzuiliwa kwa siku 6 zaidi Alice Auma Omondi anayetuhumiwa kuhusika kwenye kesi ya mauaji ya mtoto Keziah aliyekuwa na umri wa miaka 7.

Hakimu wa Mahakama hiyo Ivy Wasike ametoa agizo hilo baada ya afisa anayechunguza kesi hiyo Evans Baraza kuiambia Mahakama kwamba bado hawajakamilisha uchunguzi wao.

Alice Auma Omondi anayedaiwa kuwa Mamake mshukiwa mkuu wa mauaji hayo Dennis Otieno Odour kwa jina maarufu Dennis Mkikuu alikamatwa kama mshukiwa wa kwanza na kufikishwa Mahakamani tarehe 6 mwezi Mei 2026 ambapo aliagizwa kuzuiliwa kwa wiki tatu ili ashirikiane na maafisa wa polisi kumtafuta mshukiwa mkuu.

Hata hivyo wiki moja baadaye mshukiwa mkuu Dennis alikamatwa na kufikishwa katika Mahakama ya Shanzu ambapo bado anazuiliwa kufuatia kesi ya mauaji dhidi yake.

Maafisa wa DCI wanamshuku Alice kwamba anahusika kwenye kesi hiyo kwa kuharibu ushahidi huku maafisa hao wakipendekeza kwamba Alice pia anafaa kufunguliwa mashtaka baada ya uchunguzi kamili.

Kesi hiyo itatajwa tarehe 8 mwezi huu wa Juni.

Taarifa ya Teclar Yeri