Idara ya usalama kaunti ya Kilifi imethibitisha kumtia nguvuni mshukiwa wa mauaji ya mtoto msichana Keziah Matuki, aliyekuwa na umri wa miaka 7 kutoka kijiji cha Kwa Nzai eneo la Mwezang’ombe.
Naibu Kamishna wa eneo la Kilifi Kazkazini Samuel Mutisya, amesema jamaa huyo anazuiliwa na maafisa wa polisi na atafikishwa Mahakamani.
Mutisya amesema jamaa huyo ana kesi ya kujibu kuhusu mauaji ya mtoto Keziah kwani ripoti ya madaktari ya uchunguzi wa maiti, iliyonyesha wazi kwamba Keziah alinajisiwa na kisha kunyongwa kwa kuvunja shingo.
Mkuu huyo wa usalama, amesema maafisa wa idara ya upelelezi DCI wanaendelea na uchunguzi wa kuwasaka watu wengine ambao wanadaiwa kushirikiana na mshukiwa kuetekeleza unyama huo kwa mtoto Keziah.
“Ningetaka kuwahakikishia wananchi kwamba mshukiwa wa kitendo cha kinyama amekamatwa na yuko chini ya ulinzi wa polisi na uchunguzi unaendelea na atafikishwa Mahakamani”alisema Mutisya.
Mutisya pia amewataka wananchi kuwa na subiri wakati suala hilo likishughuliwa na maafisa wa polisi na kwamba wanafanya kila juhudi kuhakikisha familia ya Keziah inapata haki.
Kulingana na ripoti ya maafisa wa polisi, mshukiwa huyo anatambulika kwa jina Dennis Otieno Oduor kwa jina maarufu Dennis Mkikuu Mbobolo na ana umri wa miaka 26.
Taarifa hiyo ya polisi ya nambari 26/ ya tarehe 8 mwezi Mei mwaka huu, imebaini kwamba Dennis alijiwasilishwa mwenyewe katika kituo cha polisi cha Tauza eneo la Gora katika eneo bunge la Voi kaunti ya Taita Taveta kufuatia uchunguzi wa maafisa wa DCI.
Tayari Alice Auma Omondi ambaye anadaiwa kuwa mamake mshukiwa bado anaendelea kuzuiliwa na maafisa wa DCI katika kituo cha polisi cha Kijipwa eneo la Vipingo kaunti ya Kilifi kusaidia maafisa hao kukamilisha uchunguzi wao.
