Kundi la Mombasa Republican Council –MRC limeshinikiza idara ya usalama kuwaachilia huru wanachama wake waliokamatwa.
MRC inadai hatua hiyo inakiuka uamuzi wa Mahakama uliotambua kundi hilo kuwa halali kisheria hivyo kuendelea na harakati zake za kupigania maslahi ya eneo la Pwani.
Viongozi wa kundi hilo wakiongozwa na Msemaji wao Franklin Ngumbao wanadai wanachama wao wamekuwa wakikamatwa, kufuatiliwa na kunyanyaswa kila wanapofanya mikutano ya Amani kuhamasisha umma kuhusu ajenda yao eneo la Pwani.
Serikali ya Kenya inajua vizuri kwamba sisi tulienda Mahakamani na ikatupatia sisi haki kwamba tunaweza kujisimamia wenyewe mambo yetu bila kutatiza serikali ya Kenya, lakini bado makaratasi yako katika hewa tu, ushindi ule haujulikani na serikali ya Kenya.’alisema Ngumbao.
MRC imedokeza kuwa imewasilisha lalama zake kwenye mashirika mbali mbali ya kimataifa yakiwemo umoja wa mataifa, Umoja wa Afrika, Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa jinai ICC, pamoja na Mahakama ya kimataifa ya haki ICJ ili kupata msaada zaidi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kundi hilo Ziro Mwambodza amedokeza kuwa wamekuwa wakifuata njia za kisheria kwa muda japo madai yao hayajaangaziwa.
‘Ilipofika 2016 uamuzi ulitoka kwamba MRC madai yao yako sawa na wanafuata sheria kikamilifu, tumeendelea hivyo kufuata sheria mpaka sasa mahali tumefikia ni kwamba imetulazimu kutafuta msaada katika mashirika ya nje’ alisema Mwambodza.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
