Idara ya usalama kaunti ya Kilifi inapoendeleza mikakati ya kukabiliana na magenge ya kihalifu maarufu ‘Mawoza’, visa vya watu kuvamiwa vingali vinaendelea kushuhudiwa mjini Malindi kaunti ya Kilifi.
Kisa cha hivi punde kikiwa cha mwanaume mmoja ambaye alivamiwa na kukatwa mapanga na watu wanaoaminika kuwa “mawoza” vijana wanaoshiriki uhalifu eneo la Shela, Malindi kaunti ya Kilifi.
Taarifa zinasema kuwa mwanaume huyo alikuwa akielekea kuswaali alfajiri kabla ya kupatana na wahalifu hao, kisa ambacho kimethibitishwa na naibu Chifu eneo hilo, Nicodemus Mwayele, alipozungumza na COCO FM kwa njia ya simu kuhusu tukio hilo.

Wakaazi wanaitaka idara ya usalama kukabiliana kikamilifu na kundi la wahalifu la Mawoza kaunti ya Kilifi
Haya yanajiri, msako ukiendelezwa na kikosi maalumu cha usalama katika kaunti ya Kilifi kukabiliana na ‘MAWOZA’ huku baadhi ya wakaazi wakiibua hisia mbalimbali wakisema huenda msako huo ukasaidia kwa asilimia kubwa kuwakamata wanaojihusisha na visa hivyo ili wakabiliwe kisheria.
Wengine wamesema huenda juhudi hizo zikakosa kuzaa matunda wakidai licha ya wanaojihisha na visa hivyo kakamatwa huwa hawafikishwi Mahakamani kufunguliwa mashtaka.
Msako huo unajiri siku chache baada ya gavana wa kaunti ya Kilifi Gedion Maitha Munga’aro kuandaa kikao cha faragha na kamanda wa polisi ukanda wa pwani Ali Nuno, naibu kamishna wa eneo bunge la Kilifi Kaskazini Samuel Muinde Mutisya, kamanda wa polisi kaunti ya Kilifi Reginald Omaria, Mbunge wa Kilifi Kaskazini Owen Baya, Mbunge wa Malindi Amina Mnyazi na wakuu wengine wa usalama kaunti ya Kilifi.
Taarifa ya Janet Shume
